Biashara Huria Ndiyo Sera Bora

Mfumo wa ulindaji dhidi ya ushindani unaendelea kujiimarisha. Kwa kawaida sera hii ni hatari na ya kijinga; lakini ni hatari zaidi katika nyakati za matatizo ya kiuchumi, wakati inatishia kuharibu uchumi wa dunia. Dhana ya kipekee ya ulindaji dhidi ya ushindani ni kuwa ufanisi wa taifa unaongezeka wakati serikali inawapa wazalishaji wenyeji uwezo wa ukiritimba. Karne za tafakari za kiuchumi, uzoefu wa kihistoria na utafiti wa madhubuti  zimedhihirisha mara kwa mara  dhana hiyo ni potofu. Ulindaji dhidi ya ushindani unasababibisha umaskini, wala sio ufanisi. Ulindaji dhidi ya ushindani “haulindi”  viwanda na nafasi za kazi za wenyeji; unaharibu kwa kudhuru viwanda vinavyouza bidhaa nje ya nchi na pia vile viwanda vinavyotegemea bidhaa zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi.  Upandishaji wa bei za chuma kwa “kulinda” kampuni za vyuma nchini unaongeza tu gharama ya uundaji magari na bidhaa zingine nyingi zinazoundwa na chuma. Ulindaji dhidi ya ushindani ni mchezo wa kijinga.

Lakini ukweli kuwa ulindaji dhidi ya ushindani unaharibu utajiri, si matokeo yake yaliyo mabaya zaidi. Ulindaji dhidi ya ushindani unatatiza amani. Hii ndiyo sababu tosha kwa watu wote wenye heri njema, marafiki wote wa ustaarabu, kuzungumza kwa sauti na msisitizo dhidi ya utaifa wa kiuchumi, itikadi za migogoro iliyojikita katika misingi ya kijinga na kutekelezwa na ulindaji dhidi ya ushindani.

Karne mbili na nusu zilizopita, Montesquieu alitaja kuwa “amani ni zao asilia la biashara. Mataifa mawili yanayotofautiana huishilia kutegemeana; ikiwa taifa moja litakuwa na nia ya kununua, lingine litakuwa na nia ya kuuza; na hivyo muungano wao unaanzia kwa mahitaji yao ya pamoja.”

Tokeo kubwa zaidi la biashara ni amani. Biashara huimarisha amani, kwa kuwaunganisha watu tofauti tofauti katika utamaduni mmoja wa biashara- mchakato wa kila siku wa kujifunza lugha za wengine, kanuni za kijamii , sheria, matarajio, mahitaji yao, na vipawa.

Biashara hukuza amani kwa kuhimiza watu kujenga mapatano ya kunufaisha ushirika wa pamoja. Kama vile ambavyo biashara huunganisha mvuto wa kiuchumi wa Paris na Lyon, Boston na Seattle, Calcutta na Mumbai, Biashara pia huunganisha mvuto wa kiuchumi wa Paris na Portland, Boston na Berlin, Calcutta na Kopenhagen- wa watu wa mataifa yote wanaofanya biashara na wengine.

Kiasi kikubwa cha utafiti wa kina unaunga mkono pendekezo kuwa biashara huimarisha amani.

Pengine mfano wa kusikitisha wa matokeo ya kupuuza amani ni Vita Vikuu vya Pili Vya Dunia.

Biashara ya kimataifa ilianguka kwa asilimia 70%  baina ya 1929 na 1932, na sababu mojawapo ilikuwa ni ushuru wa Marekani wa 1930 uliojulikana kama ‘Smoot-Hawley” na ushuru wa kulipiza kisasi wa mataifa mengine. Mchumi wa biashara Martin Wolf anatoa maoni kuwa “kuporomoka kwa biashara kulichochea kutafutwa  kwa Autarky na Lebensraum, hasa kwa ajili ya  Ujerumani na Japani.

Vita hatari vya kutisha katika historia ya binadamu vilifuatia.

Kwa kupunguza vita, biashara huokoa maisha.

Biashara pia huokoa maisha kwa kuongeza ufanisi na kuupanua kwa watu wengi zaidi. Ushahidi kuwa biashara huria huimarisha ufanisi ni mwingi. Ufanisi huwezesha watu wa kawaida, waume kwa wake, kuishi kwa maisha yenye afya na ya muda mrefu.

Watu wakipata maisha marefu na yenye afya na amani, huingiliana na uchumi wa kimataifa na huwa na  muda mwingi wa kufurahia tamaduni tofauti tofauti ziletwazo na biashara huria. Utamaduni  unarutubishwa na michango kutoka kote duniani inayowezeshwa na biashara huria ya bidhaa na mawazo.

Bila shaka, biashara huria huimarisha ufanisi wa mali. Lakini zawadi yake kuu haipimiki kwa urahisi na pesa. Zawadi  kuu ni maisha yenye uhuru, ukamilifu na zaidi ya hayo hayatazamiwi kutiwa kovu ama kuharibiwa na ukatili wa vita.

Kutokana na hayo, sisi tuliotia saini hapa chini tunaungana pamoja kuomba serikali za mataifa yote kupuuza wito wa kibinafsi wa kuongeza vizuizi vya kibiashara unaotolewa na watu wasiokuwa na maono ya mbele. Zaidi ya hayo, tunatoa wito kwao waondoe vizuizi vilivyopo sasa vya ulindaji dhidi ya ushindani kwa biashara huria. Kwa kila serikali, tunasema: waacheni  wananchi wafurahie sio tu matunda ya mashamba yenu, viwanda na akili, bali pia ya kote duniani. Manufaa  yake ni ufanisi makubwa zaidi, maisha yenye ukwasi na furaha na baraka za amani.

RELATED ARTICLES